Mauricio Pochettino aondoka Chelsea baada ya msimu mmoja

Tom Mathinji
2 Min Read

Kocha wa Chelsea Mauricio Pochettino ameondoka katika timu hiyo kwa makubaliano ya pande zote baada ya msimu mmoja Stamford Bridge.

Klabu hii imethibitisha kuondoka kwake kupitia ujumbe siku ya Jumanne.

“Chelsea FC inaweza kuthibitisha kwamba klabu na Mauricio Pochettino wamekubaliana kuachana.” imesema klabu hiyo kwa ujumbe.

Pochettino alijiunga na Chelsea mnamo Juni 1, 2023 akitokea timu ya Paris Saint-Germain. Alitia saini mkataba wa miaka miwili akiwa na fursa ya kuongeza kwa mwaka mmoja zaidi.

Mkufunzi huyo raiya wa Argentina aliondoka PSG mnamo Julai 5, 2022 baada ya msimu mmoja. Alisaidia timu hiyo kunyakua taji la Ligue 1 msimu wa 2021/22.

Chelsea ilifanya vibaya katika kipindi cha kwanza cha msimu wa 2023/24 lakini akawaongoza kumaliza katika nafasi ya sita kwenye Ligi ya Premia. Matokeo hayo yaliimarika ikizingatiwa walimaliza msimu wa 2022/23 katika nambari ya 12.

Chelsea pia walimaliza wa pili katika Kombe la Carabao na kufika nusu fainali ya Kombe la FA.

“Asante kwa kundi la umiliki wa Chelsea na wakurugenzi wa michezo kwa nafasi,” Pochettino alisema.

“Klabu sasa iko katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika Ligi Kuu na Ulaya katika miaka ijayo.”

Wakurugenzi wa michezo wa klabu hiyo Laurence Stewart na Paul Winstanley walisema: “Kwa niaba ya kila mmoja Chelsea, tungependa kutoa shukrani zetu kwa Mauricio kwa utumishi wake msimu huu.

“Atakaribishwa tena Stamford Bridge wakati wowote na tunamtakia kila la heri katika maisha yake ya baadaye ya ukufunzi.”

Pochettino alijiunga na Chelsea kuchukua nafasi ya Kaimu Kocha Frank Lampard aliyeshikilia nafasi ya Graham Potter, aliyepigwa kalamu mnamo Aprili 2023.

Wanaotarajiwa kuchukua nafasi ya Pochettino ni makocha wa Ipswich Town Kieran McKenna, Enzo Maresca wa Leicester, Sebastian Hoeness wa Stuttgart na Michel wa Girona.

Share This Article