Maskwota walalama, wataka kugawiwa shamba la Kisiriri, Laikipia

Marion Bosire
3 Min Read

Maskwota wanataka wagawiwe shamba la ekari 2000 la Kisiriri lililo katika wadi ya Salama, eneo bunge la Laikipia Magharibi, kaunti ya Laikipia wakisema wameishi humo kwa miaka mingi sasa.

Wakizungumza na wanahabari wakati wa maandamano ya amani katika shamba hilo,watu hao walisema kwamba wanafahamu shamba hilo nambari LR-2426 linaweza kugawiwa maskwota.

Kulingana nao, mmiliki wa awali kwa jina Irene Ida Norman alifariki mwaka 1959, miaka mitatu baada ya muda wake wa kukodi shamba hilo kumalizika.

Mmoja wa maskwota hao Wilson Leshao alielezea kwamba walishangaa kuona mwekezaji wa asili ya Asia akiweka ua kwenye sehemu ya shamba hilo inayokisiwa kuwa ekari 260 hivi maajuzi.

Maskwota hao walitaka kuzungumza na Joshua Irungu ambaye wanasema anafahamu fika matatizo ambayo wamepitia kwa miaka mingi kama vile kuchomewa nyumba na usimamizi wa eneo hilo.

“Tunataka Gavana aje atupe mwelekeo la sivyo tutaandamana hadi afisi yake au makazi yake kwa sababu tunastahili kupatiwa makazi kama Wakenya wengine,” alisema Leshao.

Serikali imekuwa ikisema ardhi hiyo inamilikiwa na jamaa kwa jina George Jenning, lakini kulingana na Leshao, Jenning anamiliki shamba lililo karibu ambalo nambari yake ya usajili ni LR2425.

Mkazi mwingine wa eneo hilo Miriam Waithera amelalamika akisema hawezi kufikia stakabadhi zake muhimu baada ya sehemu ambayo nyumba yake iko kuwekwa ua na mwekezaji huyo.

“Mimi ni mmoja wa watu wa familia 66 zilizofurushwa kutoka kwa makazi yao baada ya ua kuwekwa. Niliacha stakabadhi zangu, magunia ya mahindi na mabomba ya kunyunyizia maji mashamba, vyote ambavyo vilikua ndani ya nyumba,” alisema Waithera.

Kulingana na mama huyo, wana mpango wa kushtaki mwekezaji huyo kwa kuwafurusha bila agizo lolote la mahakama kwani inasikitisha kwamba wanafurushwa kutoka makazi yao miaka 60 baada ya Kenya kujipatia uhuru na wamekaa huko kwa miaka mingi.

Moses Leng’eren alisema alizaliwa katika eneo hilo ambapo familia yake imeishi kwa miaka zaidi ya 30. Anasema naibu kamishna wa kaunti wa eneo hilo aliwaahidi kwamba watapatiwa makazi mbadala lakini hawajapata lolote.

“Tunafahamu mwekezaji wa asili ya Asia aliyesaidiwa na naibu kamishna wa eneo hilo kuweka ua kwenye shamba hili na kusababisha wengi kupoteza makazi,” alisema Leng’eren.

Veronica Moraa Gekonge ambaye pia alizaliwa katika eneo hilo anataka naibu kamishna huyo ahamishwe akisema anasaidia watu wa nchi nyingine kukalia ardhi hiyo badala ya kusaidia maskwota.

Mwenyekiti wa jamii ya Kisiriri Ibrahim Lesian anasema waliandika nyaraka kwa viongozi wote waliochaguliwa wa eneo hilo mwezi Januari mwaka huu wakitaka usaidizi lakini hawajapata jibu.

“Kama wakazi wa Kisiriri hatujapokea jibu kwa nyaraka tulizotuma za kuelezea masaibu yetu kwa Gavana Irungu, mwakilishi wa kike wa kaunti ya Laikipia bungeni Jane Kagiri na mbunge wa Laikipia Magharibi Wachira Karani,” alidai Lesian.

Alimalizia kusema kwamba wameamua kuvamia makazi ya Gavana Irungu na afisi yake watakapokaa hadi achukue hatua kuhusiana na matatizo yao.

Share This Article