Wakuu wa mashirika yote makubwa ya Umoja wa Mataifa, UN wametoa taarifa ya pamoja wakitoa wito wa “kusitishwa mapigano mara moja kwa sababu za kibinadamu” wakisema “imetosha”.
“Kwa karibu mwezi mmoja, dunia imekuwa ikitazama hali inayoendelea nchini Israel na eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu kwa mshtuko na hofu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu waliopoteza maisha yao na kusambaratika kwa hali ya kawaida,” wasimamizi hao wa Umoja wa Mataifa wanasema.
Wakuu wa mashirika yakiwemo UNICEF, WHO, Mpango wa Chakula Duniani – pamoja na mashirika ya misaada kama vile Save the Children – walielezea hasara “ya kutisha” ya maisha kwa pande zote mbili, na kutaka kuachiliwa bila masharti kwa mateka waliochukuliwa na Hamas wakati wa shambulizi lake la Oktoba 7 .
Taarifa hiyo inaendelea:
“Hata hivyo, mauaji ya kutisha ya raia wengi zaidi huko Gaza ni hasira, kama vile kuwanyima Wapalestina milioni 2.2 kupata chakula, maji, dawa, umeme na mafuta.”
Taarifa hiyo inaongeza kuwa watu 88 wanaofanya kazi UNRWA, shirika linalowasaidia wakimbizi wa Kipalestina, wameuawa tangu Oktoba 7, idadi kubwa zaidi ya vifo vya wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa “kuwahi kurekodiwa katika mzozo mmoja”.