Marekani imetoa ushauri kwa raia wake dhidi ya kutembelea baadhi ya maeneo nchini Kenya.
Kwenye ushauri huo uliotolewa leo Jumanne, nchi hiyo imehusisha hatua hiyo na uhalifu, ugaidi, maandamano ya raia na visa vya utekaji unyara inavyodai vimeshamiri humu nchini.
Kulingana na ushauri huo, kuna hatari kubwa ya kuyatembelea maeneo hayo yanayoongozwa na mitaa ya Eastleigh na Kibera iliyopo katika jiji kuu la Nairobi.
Marekani inasema mitaa hiyo imetawaliwa na uhalifu na visa vya utekaji nyara.
Maeneo mengine ambayo raia wa Marekani wametakuwa kuepuka kuyazuru ni kaunti za Garissa, Wajir na Mandera zilizo kwenye mpaka kati ya Kenya na Somalia.
Kaunti nzingine ambazo raia wa Marekani wametakiwa kuepuka kutembelea kutokana na ugaidi na visa vya utekaji nyara ni Tana River na maeneo ya pwani yaliyopo kaskazini mwa mji wa Malindi.
Raia wa Marekani pia wametakiwa kutotembelea kaunti ya Pokot Magharibi na magharibi mwa kaunti ya Turkana kutokana na wizi wa ng’ombe, na baadhi ya maeneo ya kaunti za Marsabit na Turkana yaliyo ndani ya kilomita 50 kutoka kwenye mpaka wa Ethiopia kutokana na uvamizi wa kuvuka mpaka.
Kulingana na ushauri huo, uhalifu wa vurugu kama vile uporaji kwenye magari, kuvamiwa kwa watu na kuwaibia, uvamizi wa nyumbani na utekaji nyara ni visa vinavyoweza kutokea wakati wowote.
Katika kutoa ushauri huo, Marekani pia inasema mashambulizi dhidi ya maeneo ya umma kama vile majengo ya serikali, shule na maeneo ya kuabudu yamekuwa yakifanyika bila maonyo yoyote.
Aidha, inaongeza kuwa maandamano na migomo ya wafanyakazi kimekuwa kitu cha kawaida nchini Kenya, hali inayoweza kuwa hatarishi.