Seneta wa kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago na wenzake wawili waliokamatwa jana Jumatano kwa tuhuma za kufuja pesa za hazina ya elimu wameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 2, mdhamini wa kiasi sawa au dhamana ya pesa taslimu ya shilingi laki 5 kila mmoja.
Watatu hao Mandago, Joshua Lelei na Mishack Rono walifikishwa mahakamani leo asubuhi ambapo walikabiliwa na shtaka la kufanya njama ya kuiba shilingi bilioni 1.1 kutoka kwa akaunti moja katika benki ya KCB mjini Eldoret.
Jina la usajili la akaunti hiyo ni “Uasin Gishu Education Trust Fund” ambapo wazazi walikuwa wakiweka pesa ambazo zingetumika na serikali ya kaunti hiyo kusafirisha wanao hadi Finland na kuwasajili kwenye vyuo huko.
Kulingana na stakabadhi za kesi hiyo, uhalifu huo ulitekelezwa kati ya tarehe 1 mwezi Machi na tarehe 12 mwezi Septemba mwaka 2021.
Mandago ambaye awali alihudumu kama gavana wa kaunti ya Uasin Gishu na wengine walikamatwa jana Jumatano baada ya mahakama moja ya Nakuru kutoa kibali cha kuwakamata. Mshukiwa wa nne Joseph Maritim kwa sasa yuko nje ya nchi.
Wiki jana, Mandago na wenzake walihojiwa na maafisa wa kitengo cha upelelezi wa jinai ambao wanachunguza ulaghai huo wa mpango wa elimu nchini Finland na Canada.