Mtangazaji mkongwe Leonard Mambo Mbotela jana Jumapili aliandaliwa karamu ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Mtangazaji huyo wa zamani wa KBC aliandaliwa karamu hiyo na muungano wa wataalamu wa utangazaji almaarufu Association of Professional Broadcasters-KE.
Hafla hiyo iliandaliwa katika mkahawa wa Amara.
Mbotela ambaye anafahamika kwa kipindi chake cha “Je Huu ni Uungwana?” ametimiza umri wa miaka 84.
Waliohudhuria ni watu wa familia yake, wanachama wa chama hicho cha wataalamu wa utangazaji akiwemo Dkt. Ezekiel Mutua aliyeteuliwa hivi maajuzi kama mtunzi wa chama hicho.
Dkt. Mutua alichapisha picha za tukio hilo kwenye akaunti yake ya Facebook ambapo alimmiminia sifa Mbotela na kukumbuka kazi zake kama vile kipindi cha Je Huu ni Uungwana, utangazaji wa mpira na huduma katika kitengo cha utangazaji cha Rais Moi.
Mkurugenzi huyo mtendaji wa shirika la hakimiliki za muziki nchini, MCSK alihimiza serikali kubuni mpango thabiti wa kuwaenzi watangazaji wa zamani ili kuhakikisha wanaishi maisha mazuri hata baada ya kustaafu.
“Mpango wa kuwapa fedha kama ule wa wanamichezo wanaoshinda nishani za fedha katika mashindano ya kimataifa unafaa kuanzishwa kwa ajili ya watangazaji wa zamani ambao walipeperusha bendera ya nchi na kuhimiza maadili mema kitaifa,” alipendekeza Dkt. Mutua.
Tunamtakia Mzee Mambo kila la kheri.