Makala ya 34 ya kipute cha kuwania kombe la Afrika AFCON nchini Ivory Coast yamezua viroja, huku timu zilizopigiwa upato kutwaa ubingwa zikibanduliwa katika hatua ya makundi wakati timu hafifu zikifuzu kwa hatua ya mwondaoni.
Baadhi ya miamba ambao tayari wametumuliwa mashindanoni ni mabingwa mara nne wa AFCON Ghana -Black Stars, ambao walitoka sare mbili na kupigwa mechi moja katika michuano ya kundi B.
Pia wenyeji Ivory Coast ambao wangali kwenye dua ya kuona kama walifuzu kwa raundi ya 16 bora, licha ya kumaliza katika nafasi ya tatu kundini A baada ya kusinda mchuano mmoja pekee.
Mabingwa wa mwaka 2019 Algeria pia kwa makala ya pili mtawalia wametimuliwa mashindanoni katika hatua ya makundi wakiwa na alama mbili pekee kufuatia kutoka sare mbili na kushindwa mchuano mmoja.
Timu zilizozua miujiza hadi sasa ni Equatorial Guinea, ambao waliongoza kundi A kwa pointi 7 kufuatia sare moja na kushinda miwili.
Nzalang Internaciaonal wanavyojulikana Equtorial Guinea,wamepangiwa kumenyana na Guinea katika raundi ya 16 .
Blue Sharks wa Cape Verde walifanikiwa kuongoza kundi B wakishinda mechi mbili na kutoka sare moja na wamepangwa dhidi ya Mauritania katika awamu ya 16 bora.
Msumbiji ukipenda Mambas ambao wamebanduliwa mashindano pia walijituma wakilazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Misri, na Ghana mtawalia ingawa hawakupewa nafasi ya kuzoa pointi kabla ya kuanza kwa mashindano.
Gambia ,maarufu kama Scorpions waliyaaga mashindano lakini waliandikisha historia ya kufunga mabao mawili ya kwanza katika AFCON wakiwasukumua Cameroon hadi sekunde za mwisho kabla ya kupoteza mchuano wa mwisho.
Katika kundi D Mauritania walisajili ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya miamba Algeria, likiwa goli la kwanza katika hsitoria yao ya AFCON na kufuzu kwa raundi ya 16 bora kwa mara ya kwanza.
Lions of Chinqueti wanavyojulikana waliamaliza katika nafasi ya tatu.
The Palancas Negras ya Angola waliandikisha ushindi wa kwanza katika historia ya AFCON, wakishinda mechi mbili dhidi ya Burkina Faso na Mauritania na kuongoza kundi D kwa alama saba.
Brave Warriors ya Namibia walirekodi ushindi wa kwanza dhidi ya miamba Tunisia, na kutoka sare na Mali huku wakifuzu kwa raundi ya 16 bora kwa mara ya kwanza.
Mechi za mwondoano wa 16 bora zitaanza rasmi Jumamosi na kukamilika Jumanne ijayo.