Siku kadhaa baada ya Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala kuvuliwa wadhifa huo, sasa amesitisha kimya chake na kusema kuondolewa kwake kulitekelezwa kinyume cha sheria.
“Kuondolewa kwangu kama Katibu Mkuu wa chama cha UDA kulikiuka sheria, hakukuzingatia haki na kulikiuka katika ya chama na mchakato unaopaswa kufuatwa,” alisema Malala katika mkutano na wanahabari leo Alhamisi.
Huku akitaja kutimuliwa kwake kuwa mapinduzi ya ndani ya chama, Malala alisema hakabiliwi na mashtaka yoyote ambayo yanahalalisha kuondolewa kwake, akilalamika kuwa hakupewa nafasi ya kujitetea.
“Kuondolewa kwangu katika wadhifa huo hakukutokana na kulemewa kwangu kuongoza chama hicho, lakini ni njama iliyopangwa na baadhi ya maafisa wa chama hicho,” aliongeza Malala.
Malala alisema amewasilisha ombi la kupinga kuondolewa kwake kama katibu mkuu kwa msajili wa vyama vya kisiasa, akitamtaka asitishe mchakato wa kumteua mrithi wake.
Alisema chama hicho kitakapoandaa uchaguzi wa kitaifa jinsi kilivyoagizwa na msajili wa vyama vya kisiasa, atatetea wadhifa wake wa Katibu Mkuu wa UDA.
UDA imemteua aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar kuwa kaimu Katibu Mkuu wa chama.