Viongozi wawili waandamizi wa wanajihadi wameuawa katika operesheni ya pamoja na vikosi vya kikanda katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado nchini Msumbiji, jeshi linasema.
Mmoja wao alikuwa Abu Kital ambaye “alishikilia wadhifa wa naibu kamanda wa operesheni za kundi la Ahlu-Sunnah wal Jama`a (ASWJ)”, taarifa ya jeshi ilisema.
Mwingine alikuwa Ali Mahando, ambaye pia alishika wadhifa wa juu katika kundi hilo.
Jeshi la Msumbiji na vikosi vya washirika, ikiwa ni pamoja na wanajeshi wa Rwanda na ujumbe wa kijeshi kutoka kambi ya kikanda ya kusini mwa Afrika ya Sadc, wamekuwa wakiendesha operesheni katika jimbo hilo lililoathiriwa na wanajihadi.
Msumbiji imekuwa ikipambana na waasi wenye uhusiano na kundi la Islamic State tangu Oktoba mwaka 2017.
Zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao huku wengine zaidi ya 4,000 wakiuawa katika kipindi hicho.