Majina ya walalamishi katika kesi ya Diddy yafichuliwa

Jaji aliagiza majina ya watatu hao yafichuliwe kwa mawakili wa Diddy pekee.

Marion Bosire
1 Min Read
Cassie Ventura

Waendesha mashtaka katika kesi inayomkabili mwanamuziki Sean ‘Diddy’ Combs wamefichua majina ya walalamishi watatu wa kesi hiyo lakini majina hayo yamepatiwa mawakili wa Diddy pekee.

Kulingana na ombi alilowasilisha mahakamani Diddy Machi 6, 2025, mwanamuziki huyo alitaka kufahamishwa kuhusu utambuzi wa walalamishi watatu walioorodheshwa na serikali katika hati za kesi hiyo.

Jaji alidurusu ombi hilo na kuamuru afisi ya wakili wa serikali katika wilaya ya kusini mwa New York kutoa majina hayo kwa mawakili wa Diddy kufikia Machi 10, 2025.

Watetezi hao wa Diddy wanasema wanahitaji muda wa kutosha kujiandaa kwa kesi hiyo itakayoanza kusikilizwa mwezi Mei mwaka huu, na katika kesi hiyo walalamishi wanatambuliwa tu kwa nambari 1, 2 na 3.

Maagizo ya jaji yalielekeza kwamba majina ya walalamishi yatolewe tu kwa mawakili lakini tayari watu wamekisia kwamba mlalamishi wa kwanza ni Cassie Ventura,  kwa sababu wamemhusisha na video iliyochapishwa na CNN ya kuonyesha Diddy akimpiga kwenye hoteli fulani.

Mawakili hao wamesema pia kwamba walalamishi nambari 2 na 3 walikuwa wapenzi wa awali wa Diddy na kwamba kila kilichofanyika kati yao na Diddy walikubaliana na wala sio kulazimishwa.

Website |  + posts
Share This Article