Mahakama yatupilia mbali mgao wa nafasi za ajira Bangladesh

Marion Bosire
2 Min Read
Mahakama ya upeo, Bangladesh

Mahakama moja nchini Bangladesh imetupilia mbali migao ya nafasi za ajira serikalini ambayo ilikuwa imesababisha maandamano yenye vurugu kote nchini humo.

Maandamano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 100.

Thuluthi moja ya nafasi za ajira serikalini ilikuwa imetengewa jamaa za wanajeshi waliopigania uhuru wa Bangladesh kutoka kwa Pakistan mwaka 1971.

Sasa mahakama imeamua kwamba ni asilimia 5 tu ya nafasi hizo inafaa kutengewa jamaa za wanajeshi hao na waziri wa masuala ya sheria Anisul Huq amesema serikali itatekeleza agizo hilo la mahakama katika muda wa siku chache.

Huq amekanusha pia ripoti kwamba waziri mkuu wa nchi hiyo Sheikh Hasina ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka 2009 ameshindwa kudhibiti Bangladesh.

Waziri huyo analaumu upinzani kwa kushirikiana na waandamanaji kuharibu ishara za maendeleo nchini Bangladesh, huku baadhi ya waandamanaji waliohojiwa na wanahabari wakiapa kuendelea na maandamano hadi serikali ichukue hatua.

Nusrat Tabassum mmoja wa waandalizi wa maandamano alisema kwamba malalamishi yao yanalenga serikali kuu na hadi matakwa yao yatekelezwe maandamano yataendelea kote nchini humo.

Wanafunzi wanaoandamana wanataka pia haki kwa wenzao ambao wameuawa kwenye maandamano, kuachiliwa kwa waliokamatwa, kurejeshwa kwa mtandao na kujiuzulu kwa mawaziri fulani.

Barabara za mji mkuu wa Bangladesh Dhaka, zimesalia kuwa mahame kufuatia kafyuu iliyowekwa ila maandamano yanazuka mara kwa mara hata baada ya uamuzi huo wa mahakama ya upeo.

Mahakama imeamua kwamba asilimia 93 ya fursa za ajira serikalini zitolewe kwa waliohitimu, asilimia 5 ziwekewe jamaa za wanajeshi wa zamani na asilimia 2 iliyosalia ziwaendee watu wa makundi yaliyotengwa.

Website |  + posts
Share This Article