Mahakama Kuu imetoa agizo la kuzuia kuteuliwa kwa mrithi wa Rigathi Gachagua aliyebanduliwa madarakani kama Naibu wa Rais jana Alhamisi.
Gachagua alitimuliwa jana Alhamisi baada ya Maseneta kuidhinisha mashtaka 5 kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake.
Hata hivyo, kupitia mawakili wake, Naibu huyo wa Rais wa zamani amepata agizo linalozuia kuteuliwa kwa mrithi wake hadi Oktoba 24 baada ya kuwasilisha mahakamani kesi ya kupinga kufurushwa kwake.
“Kwamba kwa wakati huu, kutokana na masuala yaliyoibuliwa katika kesi hiyo na udharura uliodhihirshwa, agizo linatolewa likizuia utekelezaji wa azimio la Seneti kumtimua mshtaki, Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya, ikiwa ni pamoja na kuteua mrithi wake hadi Oktoba 24, 2024 wakati kesi hiyo itakapotajwa mbele ya jopo lililoteuliwa na Jaji Mkuu kwa maagizo na hatua mwafaka zitakazofuata,” amesema Jaji Chacha Mwita katika uamuzi wake leo Ijumaa.
Agizo hilo linakuja wakati Bunge la Kitaifa limeidhinisha uteuzi wa Prof. Kithure Kindiki kuwa Naibu wa Rais.
Wabunge 236 walipinga kura leo Ijumaa mchana kuunga mkono uteuzi wa Prof. Kindiki katika hatua ambayo inatoa mwanya wa kuapishwa kwake kumrithi Gachagua.
Haijabainika ikiwa mchakato wa kumuapisha Prof. Kindiki kuwa Naibu Rais utaendelea mbele au la.