Mahakama kuu ya Kenya imekataa kuondoa uamuzi wa kusitisha kutekelezwa kwa sheria ya fedha ya mwaka 2023.
Jaji wa Mahakama kuu Mugure Thande, alitoa uamuzi kwamba waliowasilisha kesi hiyo wana kesi akiongeza kwamba ikiwa uamuzi huo utasitishwa, wananchi wataendelea kuathirika.
Jaji huyo aliagiza kwamba faili hiyo ipelekwe kwa jaji mkuu Martha Koome ili kubuni jopo la majaji watatu wa kusikiza na kuamua kesi hiyo.
Thande amesema kufutilia mbali agizo hilo ni kinyume cha haki za wananchi kuhusiana na kesi hiyo, akisema wananchi watakabiliwa na changamoto kuhusiana na sheria zilizofanyiwa marekebisho.
Uamuzi huo unafuatia kesi iliowasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah.
Serikali kupitia mawakili wake wakiongozwa na Profesa Githu Muigai, ilitaka kusitishwa kwa agizo hilo la mahakama.