Agizo la kaimu Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja la kupiga marufuku maandamano dhidi ya serikali, limebatilishwa na Mahakama Kuu.
Kupitia kwa taarifa tarehe Julai 17, 2024, kaimu Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, alipiga marufuku maandamano Jijini Naairobi akisema hatua hiyo inalenbga kuhakikisha usalama unadumishwa Jijini.
Huku akitoa uamuzi katika kesi iliyowasilishwa na taasisi ya Katiba Institute, Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye, alisitisha agizo hilo la Kanja hadi kesi hiyo itakapo sikilizwa na kuamuliwa.
Taasisi ya Katiba ilipinga agizo la Inspekta huyo Jenerali wa polisi ikidai kuwa inakiuka haki ya wananchi ya kuandamana kwa amani bila silaha.
Aidha Mahakama sasa imemzuia Inspekta Jenerali wa polisi na huduma ya taifa ya polisi kutekeleza agizo la marufuku dhidi ya maandamano.
Kanja alikuwa amewaonya wananchi dhidi ya kujihusisha kwenye maandamano yaliyokuwa yameitishwa leo Alhamisi, akisema polisi wamepokea habari za kijasusi kwamba makundi ya wahuni yamepanga kutumia maandamano hayo kusababisha uharibifu.