Maeneo yaliyo katika hatari ya kuwa na mafuriko yatambuliwa

Maeneo hayo yanajumuisha katikati mwa jiji la Nairobi, Globe, Gikomba, na Eastleigh.

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali imetambua maeneo ambayo yako katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na mafuriko katika kaunti ya Nairobi. 

Kaunti hiyo imeathirika na mafuriko kwa kiwango kikubwa.

Utambuzi huo unajiri saa chache baada ya mafuriko kusababisha uharibifu kwa mara ya pili juzi Jumamosi usiku katika maeneo mbalimbali ya Nairobi.

Mpango wa kunadhifisha mito ya Nairobi ndio ulitumika katika kutambua maeneo hayo ambayo ni pamoja na Kiambiu, Dandora, Kariobangi, Kayole, Komarock na Njiru. Maeneo mengine ni Ruai, Mwiki, Donholm, Savannah, Tassia, na Fedha katika eneo la Nairobi Mashariki.

Magharibi mwa Nairobi, maeneo yaliyotambuliwa ni Madaraka, Nairobi West, Lang’ata, Kawangware, Kangemi, Lavington, Westlands, Parklands, Kitisuru, Spring Valley, Kileleshwa na Chiromo.

Nairobi Kaskazini ni maeneo kama Mathare, Korogocho, na Lucky Summer kwenye mto Mathare, huku maeneo ya Kilimani, Kibera, South C, South B, Mukuru Kwa Reuben, na Mukuru Kwa Njenga yakitambuliwa huko Nairobi Kusini.

Eneo la katikati mwa jiji la Nairobi, Globe, Gikomba, Eastleigh na eneo la viwandani pia yalitajwa.

Rais William Ruto amewahakikishia Wakenya kwamba serikali imejitolea kikamilifu kushughulikia athari za mvua ya masika.

Kulingana naye, kamati maalum ya maafisa kutoka vitengo mbalimbali imebuniwa ili kuhakikisha ushirikishi wa shughuli za dharura jijini Nairobi na maeneo mengine yaliyoathirika nchini.

Aidha, alisema asasi husika zinatekeleza shughuli za uokoaji na kukarabati mifumo ya kuondoa taka na maji na kuhakikisha urejesho wa barabara katika sehemu zilizokumbwa na mafuriko.

Share This Article