Madereva wa mabasi Uganda wasimamisha mgomo

Ulisimamishwa baada ya wawakilishi wa vyama vya madereva kujitenga nao na kuunga mkono mazungumzo na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Marion Bosire
2 Min Read

Madereva wa mabasi nchini Uganda wanaripotiwa kusimamisha mgomo waliokuwa wamepanga kuanzisha hii leo, kuruhusu majadiliano.

Mgomo huo wa kitaifa ambapo madereva wangeketi chini bila kufanya kazi, ulisimamishwa kufuatia makubaliano ya dharura ya kufanya mazungumzo na serikali, polisi na waendeshaji hao wa mabasi.

Hatua hiyo iliyotishia kulemaza usafiri wa umma kote nchini Uganda, ilisitishwa baada ya wawakilishi wa Chama cha Madereva wa Mabasi Uganda, UBDA na Bus Drivers Advocacy Forum Uganda Limited, BDAFU, kujitenga na mgomo huo na kuunga mkono mazungumzo na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Kutokana na uamuzi huo, huduma za mabasi nchini Uganda zinaendelea kama kawaida hii leo.

Madereva wanapinga kanuni kali za usalama, hasa gharama kubwa za kupata beji za magari ya huduma za umma na sharti la kuzihuisha kila mwaka.

Wanataka pia mafunzo ya lazima ya kurejelea maarifa ya udereva, yanayohitajika kila baada ya miezi 24 yakomeshwe, wakisema gharama zake zinawaongezea mzigo wa kifedha.

Aidha, madereva wanataka mazungumzo kuhusu maslahi duni ya wafanyakazi, mishahara midogo na adhabu kali zinazotolewa katika utekelezaji wa sheria za barabarani.

Vyama vya madereva vimeonya kuwa utulivu wa muda mrefu utategemea matokeo ya mazungumzo ya pande tatu yanayotarajiwa leo, hasa iwapo yataleta maboresho halisi ya mazingira ya kazi na kupunguza masharti ya udhibiti.

Share This Article