Weasel ataka muziki wake uondolewe kwenye orodha ya UPRS

Hii ni baada ya kutoridhishwa na pesa alizolipwa kama mrabaha.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Weasel Manizo amewasiliana rasmi na chama cha hakimiliki za watumbuizaji nchini Uganda, UPRS akikitaka kiondoe muziki wake kwenye orodha ya kazi za sanaa inazosimamia.

Weasel ambaye jina lake halisi ni Douglas Seguya Mayanja, anaaminika kuafikia uamuzi huo kufuatia pesa alizolipwa kama mrabaha na UPRS ambazo ni shilingi 285,498 pesa za Uganda, sawa na shilingi elfu 10 pesa za Kenya.

Msanii huyo anashangaa wasanii chipukizi walipata pesa ngapi iwapo wasanii wakubwa kama yeye wanalipwa pesa hizo kwa kazi zao zote katika muda wa miezi 18.

Analaumu UPRS kwa usimamizi mbaya, ukosefu wa uwazi na kile anachokidhania kuwa ulaghai katika kusimamia mrabaha wa muziki wa kampuni yake ya Goodlyfe music.

Pesa alizolipwa msanii huyo, anasema haziendani na ithibati za jinsi muziki wake ulitumika kwenye vituo vya redio, runinga, mikutano ya hadhara, matumizi ya kibiashara na majukwaa mengine.

Katika ilani rasmi ya kisheria, Weasel anaonya UPRS kwamba iwapo itakosa kuondoa kazi zake kwenye usimamizi wake mara moja, atalazimika kuchukua hatua za kisheria.

Suala la mirabaha limekuwa tatizo sugu sio tu nchini Uganda bali pia katika nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo mashirika ya kusimamia hali miliki hulaumiwa kila mara kwa kusimamia visivyo mirabaha.

Share This Article