Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, ameagiza Huduma ya Uteuzi wa Wanafunzi Kujiunga na Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kadri nchini Kenya, KUCCPS kufungua tena mfumo wake wa maombi.
Hatua hii inalega kutoa fursa kwa wale ambao walichelewa kuwasilisha maombi yao kipindi kilichopita.
Ogamba alitangaza hilo Jumatano alipozindua rasmi matokeo ya uteuzi wa wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu na vyuo vya kadri mwaka wa masomo wa 2026/2027 katika Ukumbi wa Edge, jijini Nairobi.
Alisema watahiniwa 980,535 waliofanya mtihani wa kidato cha 4, KCSE mwaka 2025 walistahili kutuma maombi ya kujiunga na taasisi za elimu ya juu.
Kati yao, wanafunzi 268,729 walipata alama ya wastani ya C+ na zaidi, na kufuzu kujiunga na programu za shahada moja kwa moja.
Waziri huyo alisema baadhi ya wanafunzi waliokuwa wamehitimu hawakuweza kuwasilisha maombi yao kutokana na sababu mbalimbali, hali iliyosababisha serikali kutoa fursa nyingine kupitia kufunguliwa tena kwa mfumo wa KUCCPS.
Ili kuongeza uhuru wa uchaguzi na kusaidia wanafunzi kuchagua kozi zinazolingana na malengo yao ya taaluma, Ogamba pia aliongeza muda wa uhamisho kati ya vyuo vikuu kutoka wiki mbili hadi mwezi mmoja.
Aidha, alitangaza kuwa mfumo wa Maombi ya Ufadhili wa Elimu ya Juu umefunguliwa kwa waombaji wa mara ya kwanza baada ya kukamilika kwa zoezi la uteuzi.
Wanaostahiki sasa wanaweza kutuma maombi ya ufadhili wa serikali kupitia mfumo wa Bodi ya Ufadhili wa Elimu ya Juu au wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, HELB.