Taarifa ya Boniface Musotsi.
Mabingwa watetezi wa mchezo wa Raga ya wachezaji 15 kila upande baina ya shule za upili Vihiga, leo Ijumaa wamebanduliwa na shule ya wavulana ya Kakamega.
Vihiga wanasalimu amri kwenye mechi ya kanda ya Magharibi mwa nchi, iliyochezewa kwenye uga wa shaule yao.
Mabingwa hao wa mwaka 2025 walipoteza ngarambe hiyo yenye ushindani mkali baada ya kuadhibiwa kwa alama 7-0 , zilizofungwa katika kipindi cha pili.
Aidha mashabiki wa timu ya Vihiga waligadhabishwa na hatua ya wasimamizi wa mechi hiyo kuipokonya timu yao alama tano walizopata dakika za mwisho za mechi hiyo, wakiitaja kuwa isiyofaa.
Kwenye nusu fainali ya pili, Bungoma iliinyofoa Senende alama 21 kwa sufuri.
Siku ya Jumamosi, kakamega itachuana na Bungoma kwenye fainali nazo Vihiga na Senende zikabane koo kutafuta nambari ya tatu.
Mshindi wa fainali atawakilisha eneo hilo katika kipute cha kitaifa mjini kisumu mwezi ujao.