Mabanati wa Kenya, Junior Starlets watafungua kampeini ya kufuzu kwa kombe la dunia kwa wasichana chini ya umri wa miaka 17 katika mkondo wa kwanza wa raundi ya pili dhidi ya Uganda.
Pambano hilo litasakatwa katika uchanjaa wa Nakivubo mjini Kampala, kabla ya mechi ya marudio kupigwa wikendi ijayo.
Mshindi atafuzu kwa raundi ya tatu atakapokabiliana na aidha Cameroon au Ethiopia mwezi ujao kwenye raundi ya tatu.
Timu nne bora zitafiuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Morocco mwezi Oktoba mwaka huu.
Kenya ilifuzu kwa fainali hizo kwa mara ya kwanza mwaka jana katika Jamhuri ya Dominika, ilipomaliza ya tatu katika kundi lao baada ya kushinda mechi moja.
Katika mechi nyingine za raundi ya pili mkondo wa kwanza wikendi hii, Cameroon itachuana na Ethiopia, Tanzania wamenyane na Zambia, Benin dhidi ya DRC, huku Nigeria ikivaana na Afrika Kusini.
Botswana watukuwa na miadi dhidi ya Algeria nao Ivory Coast washikane mashati na Burundi, wakati Sierra Leone wakimaliza udhia na Guinea.