Wakenya wamejitokeza kwenye barabara za miji mbalimbali nchini kuandamana kulalamikia mswada wa fedha wa mwaka 2024 ambao unaendelea kujadiliwa katika bunge la taifa.
Vijana wengi almaarufu Gen Z wameripotiwa kufanya maandamano katika miji ya Nairobi, Nakuru, Kisumu, Nyeri, Nanyuki, Eldoret na Kakamega.
Wengi walionekana wakibeba mabango yaliyotoa wito kwa wabunge kupiga kura ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024 huku baadhi wakitaka mswada huo kutupiliwa mbali kabisa.
Jijini Nairobi, maafisa wa polisi walishika doria hasa nje ya majengo ya bunge kunakoendelea mjadala wa mswada huo. Maafisa wa usaama pia walionekana kushika doria katika miji mingine kunakofanyika maandamano huku waandamanaji wakitoa wito kwa maafisa hao kutowakandamiza kwani maandamano yao ni ya amani.
Awali, waandamanaji walisambaziana vituo vya kukutana katika miji mbalimbali ili kuanza maandamano na maafisa wa polisi wakatumwa kwenye vituo hivyo mapema kujaribu kuwatawanya.
Mjini Eldoret, waandamanaji walijitokeza mapema wakiwa wamebeba mabango yenye maneno ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka huu pamoja na miito kwa wabunge kuukatalia mbali.