Baraza la Vyombo vya Habari nchini, MCK limelaani vikali hatua ya maafisa wa usalama kuwanyanyaswa wanahabari waliofuatilia maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 katika maeneo mbalimbali jana Jumanne.
Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo David Omwoyo katika taarifa alisema inasikitisha kuwa wanahabari wameendelea kudhulumiwa wakati wa maandamano hayo ilhali wajibu wao wa pekee ni kulinda ya haki ya Wakenya kupata taarifa sahihi.
“Tunatoa wito kwa Mamlaka Huru ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi, IPOA na taasisi zingine za kikatiba kufanya uchunguzi na kuhakikisha wale wanaohusika wanawajibishwa,” Omwoyo alitoa wito katika taarifa.
“MCK inavipongeza vyombo vya habari kwa kujitolea kunakili na kuripoti kwa Wakenya matukio haya muhimu katika historia ya nchi yetu licha ya wenyewe kukabiliwa na hatari kubwa. Huu ndio mchango wa vyombo vya habari kwa demokrasia.”
MCK imetoa wito kwa wanahabari kuchukua tahadhari wakati wa kuangazia matukio kama hayo.
Wanahabari kadhaa walijeruhiwa wakati wakifuatilia maandamano ya jana Jumanne na baadhi kukimbizwa hospitali ili kupokea matibabu.
