Maandalizi ya sherehe za Mashujaa, yamekamilika katika uwanja wa michezo wa Kwale.
Kitengo cha KBC Digital kilizuru Uwanja huo Leo Jumamosi kupigia kurunzi maandalizi hayo, na kubainisha uwanja huo uko tayari kwa sherehe hizo kesho Jumapili.
Jumamosi alasiri bendi za muziki zilikuwa zikipiga msasa mazoezi yao, sawia na wacheza densi pamoja na kwaya zilizoalikwa.
Maafisa wa usalama walikuwa na shughuli nyingi huku wakijizatiti kuhakikisha maswala yote ya usalama yanashughulikiwa.
Huduma za dharura ikiwa ni pamoja na magari ya kuwabeba wagonjwa na ya kuzima moto, pia yaliwekwa tayari kuhakikisha visa vyovyote ya dharura vimetiliwa maanani.
Fauka ya hayo barabara zote zinazoelekea katika Uwanja huo pia zilifanyiwa ukarabati, huku taa za barabarani, zikileta mwanga wa matumaini katika kaunti hii.
Uwanja huu wa Kwale una uwezo wa kuwahifadhi watu 10,000.
Kulingana na kamishna wa eneo la Pwani Rhoda Onyancha, milango ya Uwanja huu itafunguliwa saa kumi alfajiri.