Maafisa wa utawala kupewa mafunzo ya kuwawezesha kuboresha huduma

Martin Mwanje
1 Min Read

Maafisa wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa, NGAOs watapewa mafunzo yanayokusudia kubadilisha mtazamo wao na kuboresha utoaji huduma kwa raia wanaowahudumia.  

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo amewataja maafisa hao kuwa kiungo muhimu katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika sehemu za mashinani chini ya Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu, BETA.

“Wakiwa maafisa wa kwanza wa serikali katika sehemu za mashinani, idara hii hutekeleza wajibu muhimu katika kubadilisha utoaji huduma na kuhakikisha uafikiaji wa athari ya uwekezaji uliolengwa,” amesema Dkt. Omollo katika taarifa.

“Kwa misingi hiyo, tumependekeza kuanzisha mpango wa utoaji mafunzo ya kubadilisha mtazamo kwa maafisa hawa kwa lengo la kuhakikisha wana mtazamo wa kuongoza kwa kutoa mfano wa kuigwa katika mfumo wa utawala na kuhakikisha utoaji huduma bora katika ngazi zote.”

Maafisa 30 watakaotoa mafunzo hayo tayari wameteuliwa na tayari wananolewa makali ya namna ya kuendesha shughuli hiyo.

Aidha Dkt. Omollo anasema kusudi la mafunzo hayo ni kuhakikisha maafisa hao wanatangamana vizuri na raia kwa kuelewa mahitaji na mashaka yao.

 

Share This Article