Maafisa wa Polisi wawakamata washukiwa wawili wa mauaji

Tom Mathinji
1 Min Read
Maafisa wa DCI wawakamata washukiwa wawili wa mauaji.

Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wamemkamata Cecilia Wangari Kirisa mwenye umri wa miaka  39, baada ya kuhusishwa na mauaji ya Maxwell Wamwea, yaliyotekelezwa Mei 11, 2022,  katika mtaa wa Kasarani Jijini Nairobi.

Awali kesi hiyo ilikuwa imeripotiwa katika kituo cha polisi cha Kasarani kama kifo kilichosababishwa na umma.

Hata hivyo baada ya malalamishi kuripotiwa Novemba 19, 2023, idara ya DCI ilianzisha upya uchunguzi. Baada ya kupokea matokeo ya uchunguzi, afisi ya kiongozi wa mashtaka ya umma ilipendekeza Wangari na mshukiwa mwingine ambaye angali anasakwa, wafunguliwe mashtaka ya mauaji.

Wangari alinaswa mafichoni mwake katika hoteli moja eneo la Thindigwa, kaunti ya Kiambu, na anatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Katika tukio tofauti, mshukiwa mwingine wa mauaji Martin Asembo Masemo mwenye umri wa miaka 32, alikamatwa kufuatia uchunguzi unaoendelea kuhusu mauaji ya George Njuguna Ngung’u, kilichotokea Julai 31, 2024 na mauaji ya Victoria Mumbua Moloki, yaliyotekelezwa  Septemba27, 2024.  Waathiriwa hao wawili walikuwa madereva wa teksi Mombasa na Migori mtawalia.

Masemo anaaminika kuwa mshirika wa is Edwin Kipngetich, ambaye tayari anakabiliwa na mashtaka ya mauaji katika Mahakama Kuu ya Nakuru.  Maafisa wa polisi wanatarajiwa kuwasilisha mahakamani ombi la kumzuilia zaidi mshukiwa huyo, ili kuwapa fursa ya kukamilisha uchunguzi.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *