Maafisa wa GSU wajeruhiwa baada ya gari kukanyaga kilipuzi Lamu

Marion Bosire
1 Min Read

Takriban maafisa 10 wa GSU walijeruhiwa Jumapili asubuhi wakati gari walimokuwa wakisafiria kukanyaga kilipuzi kilichokuwa kimetegwa chini ya ardhi.

Kilipuzi hicho kinakisiwa kutegwa na wanamgambo wa Al-Shabaab katika eneo la Mlima wa Faru, kati ya Pandanguo na Witu katika kaunti ya Lamu.

Naibu Kamishna wa eneo la Lamu Magharibi Gabriel Kioni alithibitisha kisa hicho kilichosibu maafisa wa GSU waliokuwa wakishika doria katika eneo hilo linalopakana na msitu wa Boni.

Kundi la maafisa wa vitengo mbalimbali ambalo limepatiwa jina la “Amani Boni” linaendeleza harakati za kufurusha wanamgambo wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha kwenye msitu huo wa Boni.

Kulingana na Kioni, maafisa waliojeruhiwa ni wa kambi ya GSU ya Pandanguo.

Baada ya tukio hilo, wanamgambo walijitokeza kujaribu kuvamia maafisa hao, jambo ambalo lilisababisha wafyatuliane risasi kwa muda.

Kundi la maafisa wa KDF na wengine kutoka kitengo maalum walifika mahali pa tukio kusaidia wenzao lakini pia walivamiwa na wanamgambo ila walifanikiwa kutuliza hali.

Tukio hilo lilijiri siku chache tu baada ya Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki kuzuru kaunti ya Lamu.

Wakati wa ziara hiyo, Kindiki alihakikishia wakazi usalama huku kukiwa na hofu ya kushambuliwa na wanamgambo wa Al-Shabaab.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *