Maafisa wa Ukusanyaji ushuru Nchini (KRA) wamenasa lori lililokuwa likisafirisha magunia 144 ya sukari kwa njia haramu, katika mpaka wa Lunga Lunga kaunti ya Kwale.
Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa wa forodha walisimamisha lori hilo lenye nambari za usajili za kigeni, na kupata sukari ambayo haikuwa imekaguliwa.
Lilipopekuliwa kwa kina, magunia 144 ya sukari ya magendo yalipatikana yakiwa yamefichwa chini ya machungwa kuepuka kulipia ushuru. Sukari hiyo inakisiwa kuwa thamani ya shilingi 1,080,000.
Kamishna wa forodha na shughuli za mpakani Dkt. Lillian Nyawanda, alisema hatua hiyo ni mojawepo wa juhudi za kukabiliana na biashara ya magendo katika mipaka ya taifa hili.
“Dereva wa lori hilo hakuwa na stakabadhi zozote kuhusu sukari hiyo,” alisema Dkt. Nyawanda.
Lori hilo pamoja na sukari hiyo, zinazuiliwa, huku uchunguzi wa asasi mbali mbali ukiendelea.