Maafisa wa DCI wawakamata washukiwa wawili wa uhalifu

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa wa uhalifu wamakatwa na maafisa wa DCI.

Washukiwa wawili wa uhalifu wamekamatwa baada ya msako mkali uliotekelezwa na maafisa wa idara ya upelelezi wa makosa ya Jinai DCI, kutoka vituo vya polisi vya Mariakani na Kaloleni.

Wawili hao Harun Kariuki mwenye umri wa miaka 33 na mshirika wake anayeaminika pia kuwa mpenzi wake Christine Nyakio Kinyua mwenye umri wa miaka 20, wanatuhumiwa kwa kupanga misururu ya visa vya uhalifu Mombasa na Mariakani.

Aidha wanahusishwa na utekaji nyara na wizi wa kimabavu mnamo Julai 24 ,2024 na kisa cha ufyetulianaji risasi Julai 17, 2024.

Baada ya kutoroka mitego kadhaa ya maafisa wa usalama, washukiwa hao baadaye walinaswa katika maficho yao mjini Samburu.

Walipatikana na vifaa vinavyoshukiwa kuwa vya wizi, ambavyo ni pamoja na simu 9 za rununu, televisheni, jenereta mbili, kipakatalishi, nambari za usajili wa pikipiki KMGB 786D na kofia ya usalama inayovaliwa na mwendesha pikipiki KMFX 866Q.

Kupitia ukurasa wa X, idara ya DCI imesema vifaa hivyo vitatumiwa kama ushahidi, huku washukiwa hao wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Share This Article