Wahalifu jana Jumatano usiku waliwaua maafisa watano wa usalama katika eneo la Elwak.
Kufuatia mauaji hayo, Waziri wa Usalama Kithure Kindiki amewataka maafisa wa usalama kukabiliana vikali na wahalifu nchini.
“Nawauliza maafisa wa usalama kukabiliana vikali na magaidi, majangili na wahalifu wengine waliojihami kwa silaha. Hakutakuwa na msamaha kwa wahalifu wanaowadhuru maafisa wetu,” alisema Kindiki wakati wa kuzinduliwa kwa kaunti ndogo ya Lokichogio, kaunti ya Turkana leo Alhamisi.
“Ili kukabiliana na visa vya ujangili kwenye barabara ya Kitale kuelekea Lodwar, katika muda mfupi ujao, tutaitaweka hifadhi ya wanyama pori ya Turkana Kusini kwenye gazeti rasmi la serikali kama eneo la uhalifu na operesheni ya kiusalama.”
Punde hilo litakapofanyika, Kindiki alisema ni maafisa wa shirika la wanyama pori nchini, KWS na wanyama pori pekee watakaoruhusiwa kwenye hifadhi hiyo.
Aliongeza kuwa watafanya upekuzi mkali kwenye hifadhi hiyo na kukabiliana vilivyo na wahalifu wanaojificha hapo.