Hisia mseto zinaendelea kutolewa kuhusiana na maafa yaliyotokea wakati wa maandamano ya Saba Saba yaliyofanyika Julai 7 humu nchini.
Watu wasiopungua 10 waliuawa wakati wa maandamano hayo huku wengine wengi wakiuguza majeraha.
Likisitisha kimya chake kuhusiana na maandamano hayo, Shirikisho la Wanawake Mawakili nchini Kenya (FIDA) limelaani mauaji hayo na kutaka wahusika kuchukuliwa hatua kali.
Akiwahutubia wanahabari leo Jumatano, mwenyekiti wa FIDA Christine Kungu hususan amekemea hulka ya maafisa wa polisi kuficha nyuso zao wakati wa maandamano hayo, hatua anayoseme inakiukika agizo la mahakama.
Kungu sasa anamtaka Inspekta Mkuu wa Polisi kuhakikisha maafisa wote waliohusika katika mauaji ya Wakenya walioandamana kwa amani wanachukuliwa hatua za kisheria.
Kadhalika, ametoa wito kwa Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi, IPOA kuharakisha uchunguzi kuhusiana na mienendo ya polisi wakati wa maandamano hayo ili waliohusika katika mauaji hayo wawajibishwe.
Wito kama huo umetolewa na viongozi wa upinzani, wakiongozwa na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, wanaodai serikali ilitumia kikosi maalum kuwakanadamiza waandamanaji kama ilivyoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini.
Upinzani umewashutumu maafisa wa polisi kwa kusababisha mauaji ya waandamanaji wakati wa maandamano siyo tu ya Saba Saba bali pia ya Juni 25.
Jana Jumanne, Jaji Mkuu Martha Koome alitoa wito kwa maafisa wa polisi kujizuia wakati wa maandamano na kuwataka kuwa mbioni kuwatenganisha waandamanaji wa amani na wahuni.
Koome alisema polisi wanapaswa nyakati zote kufanya kazi yao kwa kuzingatia sheria.