Leseni ya kuhudumu ya magari ya uchukuzi ya Super Metro yasimamishwa

Magari 15 ya kampuni hiyo hayana vyeti halali vya ukaguzi na leseni za magari mengine 8 za kuhudumu barabarani zimepitwa na wakati.

Marion Bosire
2 Min Read

Mamlaka ya uchukuzi na usalama barabarani – imesimamisha leseni ya kuhudumu ya magari ya uchukuzi wa abiria ya kampuni ya Super Metro, baada ya kampuni hiyo kukosa kuafikia masharti ya usalama wa abiria na watumizi wengine wa barabara.

Uchunguzi wa kina uliotekelezwa katika mifumo ya Super Metro ulifichua ukiukaji wa kanuni mbali mbali kama vile vyeti vilivyopitwa na wakati vya ukaguzi wa magari pamoja na leseni za kuhudumu za magari kadhaa.

Kati ya magari 523 ya kampuni hiyo, 15 hayana vyeti halali vya ukaguzi na leseni za magari mengine 8 za kuhudumu barabarani zimepitwa na wakati.

Kando na hayo, magari 171 hayana vifaa vya kudhibiti kasi, huku 109 yakipatikana yakitumia kasi ya zaidi ya kilomita 80 kwa saa, kasi ambayo ni halali nchini.

Kampuni ya Super Metro inadaiwa pia kukiuka sheria za leba kwa kuajiri madereva ambao hawajahitimu na kukosa kuwapa waajiriwa mafao stahiki inavyohitajika kisheria.

Kutokana na hilo, leseni za madereva 64 wa kampuni hiyo zimesimamishwa baada yao kukosa kupita majaribio waliyofanyiwa Machi 10, 2025.

Ili kurejeshewa leseni, kampuni ya Super Metro ni lazima itekeleze kikamilifu mabadiliko kadhaa kama vile ukaguzi wa magari, kujaribiwa upya kwa madereva na kuhakikisha inatimiza masharti ya usalama na sheria za ajira.

Kampuni hiyo inahitajika pia kuwapa mafunzo ya usalama madereva wake wote.

Wakenya wamehimizwa kutoabiri magari ya Super Metro kwa muda usiojulikana huku NTSA ikionya kwamba magari ya kampuni hiyo yatakayopatikana yakiendeleza kazi wakati wa kusimamishwa kwa leseni yatakamatwa.

Haya yanajiri kufuatia kisa cha hivi maajuzi ambapo mmoja wa wahudumu wa magari ya Super Metro aliripotiwa kumtupa abiria nje ya gari likiendelea na mwendo. Jamaa huyo alijeruhiwa vibaya na baadaye akafariki, suala lililoghadhabisha umma.

Website |  + posts
Share This Article