Lady Jaydee atuzwa kwa mchango wake kwa muziki wa Bongo Fleva

Marion Bosire
2 Min Read

Judith Wambura Mbibo maarufu kama Lady Jaydee alitambuliwa na tuzo za Bongo Fleva kwa waanzilishi wa aina hiyo ya muziki almaarufu Bongo Fleva Honors mwaka 2024.

Jaydee alituzwa kwa mchango wake mkubwa kwa muziki wa Bongo Fleva ambao amekuwa akiimba tangu mwaka 2000.

Hafla ya mwaka huu iliandaliwa Oktoba 25, 2024, katika eneo la Warehouse Arena jijini Dar es Salaam, waandalizi wakiwa Deiwaka na King’s Music.

Waandalizi wa mvinyo aina ya John Walker ndio walikuwa wadhamini wa hafla hiyo iliyosababisha Profesa Jay kupanda jukwaani baada ya muda kufuatia kuugua kwake.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha redio cha E FM alikokwenda kupigia debe hafla hiyo, Joseph Mbilinyi almaarufu Sugu alimtaja Jaydee kuwa kiungo muhimu katika muziki wa Bongo Fleva miaka ya awali.

Sugu alielezea kwamba alipomfahamu Jaydee hakujua kwamba angeingilia muziki kwani alikuwa mtangazaji na anaridhika kuwa mmoja kati ya wasanii walioshirikiana naye kikazi.

Jaydee amekuwa kwenye ulingo wa muziki wa Bongo Fleva wa Tanzania kwa zaidi ya miaka 24 na ana albamu saba ambazo ni Machozi ya mwaka 2000, Binti ya mwaka 2003, Shukrani ya mwaka 2007, The Best of Lady Jaydee ya mwaka 2012, Nothing But The Truth ya mwaka 2013, Woman ya mwaka 2017 na 20 ya mwaka 2021.

Tuzo za wakongwe wa bongo Fleva yaani Bongo Fleva Honors zilianzishwa mwaka jana.

Jaydee sasa anaangazia maandalizi ya hafla ya kuadhimisha miaka 25 katika muziki.

Website |  + posts
Share This Article