Shirika la Huduma za Wanyamapori nchini (KWS), limefanikiwa kumnasa fisi mtoro aliyeonekana akizurura mtaani Embakasi.
KWS imethibitisha ufanisi wao kupitia ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa Facebook siku ya Jumanne.
Shirika hilo limesema lilipokea simu ya dharura kutoka kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi chuo cha ‘A’ huko Embakasi kwamba fisi huyo alionekana akizurura eneo hilo.
“Maafisa wa KWS Nairobi walipokea simu ya dharura kutoka kwa kitengo cha Huduma ya Kitaifa ya Polisi ‘A’ huko Embakasi. Mgeni asiyetarajiwa alikuwa ameonekana akizurura mtaani: Fisi!,” ilisema taarifa ya KWS.
Shirika hilo lilibainisha kuwa mafisa wake walichukua hatua mara moja na kupeleka mtego maalum wa kukamata fisi bila kumdhuru.
“Baada ya kutumia ujuzi wetu vizuri kwa uangalifu, fisi huyo alifanikiwa kukamatwa na kuwa tayari kurejeshwa katika makazi yake halali,” KWS lilisema.
KWS ilisafirisha fisi huyo kwa usalama hadi hifadhi ya Wanyamapori ya Kitaifa ya Nairobi na kumwachilia huru.
“Dhamira hii yenye mafanikio haiangazii tu kujitolea na utaalamu wa maafisa wetu, lakini pia inasisitiza dhamira yetu ya kuishi pamoja kwa amani kati ya wanyamapori na jamii,” liliongeza KWS.
KWS lilihimiza umma kuwasiliana nao ikiwa watakutana na matukio yoyote ya wanyamapori.
“Tuwasiliane kupitia laini yetu ya 24-7 Bila Malipo kwa 0800 597 000 au WhatsApp 0726 610509 kwa uingiliaji kati wa haraka,” lilisema shirika hilo.