Kunle Remi ashangaza wengi kwa kuchagua mpambe wa kike kwa harusi yake

Marion Bosire
1 Min Read
Kunle na Bimbo kwenye harusi yake ya kitamaduni

Mwigizaji wa Nigeria Oyekunle Opeyemi Oluwaremi maarufu kama Kunle Remi alifunga ndoa na kilichoshangaza wengi ni hatua yake ya kuwa na mpambe wa kike.

Kunle aliamua kumteua mwigizaji mwenza Bimbo Ademoye kuwa mpambe wake kwenye harusi yake ambayo ilikuwa ya awamu mbili, ya kitamaduni na ya kanisani.

Uhusiano wa kirafiki kati ya Kunle na Bimbo unaaminika kukita mizizi baada yao kuigiza kama mume na mke kwenye filamu “Anikulapo” ya mwaka 2022.

Kwenye harusi ya kitamaduni ya Kunle na mkewe Tiwi, Bimbo alivaa mavazi sawia na wapambe wa kiume ambayo yalikuwa mavazi ya kitamaduni ya Nigeria ya rangi nyeupe na vazi la kichwa la rangi ya zambarau.

Wakati wa harusi ya Tiwi na Kunle ya kanisani, Bimbo alivaa suti ya rangi nyeusi na shati jeupe sawa na wapambe wa kiume wa harusi hiyo.

Bimbo alichapisha video fupi inayomwonyesha akisakata densi na Kunle pembezoni mwa harusi yake ya kitamaduni na kuandika, “Ndugu yangu amepata jiko. Majukumu ya mpambe. Nina furaha sana.”

Siku ya harusi ya kanisani Bimbo alichapisha video inayomwonyesha akivaa na akiingia kwenye gari kuelekea kanisani akisema alikuwa anaendeea na majukumu ya mpambe kwenye harusi ya ndugu yake na mkewe.

Share This Article