Uncle T aitwa BASATA alivyoagiza Gwajima

Marion Bosire
1 Min Read
Anko T

Mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania anayejiita Uncle T, ameitwa kufika mbele ya Baraza la Sanaa la Taifa BASATA kama alivyoagiza waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, Dkt. Dorothy Gwajima.

BASATA imechapisha bango la wito kwa Uncle T kwenye akaunti rasmi ya Instagram na anatakiwa kufika huko bila kukosa kesho Jumatatu Oktoba 6, 2025 saa nne asubuhi.

Waziri Gwajima alichukua hatua hiyo ili jamaa huyo aweze kujieleza kufuatia tuhuma mbalimbali kutoka kwa jamii zinazodai kuwa anakiuka maadili.

Gwajima alitoa agizo hilo jana Oktoba 4, 2025 kupitia ukurasa wake wa Instagram, ambapo alielezea kwamba wanamitandao kadhaa wamemtumia hoja nyingi kuhusu shughuli za mtu huyo kwamba maudhui yake hayana maadili na yanaharibu vizazi.

Aidha, Waziri Gwajima alisema alipitia ukurasa wa Instagram wa mtu huyo akajionea machapisho mbalimbali ikiwemo matangazo yanayomwonyesha akivaa nguo za kike licha ya yeye kuwa mwanaume.

Alifafanua kuwa suala hilo linapaswa kupata mwongozo kutoka kwa wizara ya utamaduni na sanaa kwa kuwa maadili ni zao la mila na tamaduni, na Wizara hiyo ndiyo yenye vyombo vya kisheria vinavyosimamia wasanii, filamu na kazi za sanaa kwa jumla.

Website |  + posts
Share This Article