Kundi la muziki Blu*3 huenda likarejea

Marion Bosire
1 Min Read

Kuna fununu kwamba kundi la muziki la Blu*3 huenda likarejea tena miaka 13 tangu liliposambaratika.

Inaarifiwa kwamba waliokuwa wanachama wa kundi hilo Cindy Sanyu, Jackie Chandiru, na Lilian Mbabazi wanapanga tamasha ya pamoja mwakani.

Kabla ya hapo, wote watatu ambao kila mmoja sasa anaimba peke yake watatumbuiza kwenye hoteli ya Protea Marriot jijini Kampala Alhamisi Disemba 14, 2023 usiku kwenye tamasha ya kila mwezi kwa jina “Skyz Exclusive night”.

Blu*3 ni kundi ambalo lilibuniwa mwaka 2004 baada ya wanadada hao kuibuka washindi wa shindano la uimbaji la Coca Cola Popstars.

Waliandaa albamu yao ya kwanza kwa jina “Hitaji” ambayo walizindua rasmi kwenye uwanja wa Lugogo Disemba 2004, tamasha ambayo ilijaa mashabiki wao. Baadaye mwaka 2007 walizindua albamu nyingine
“Burrn”.

Sanyu ndiye aliondoka wa kwanza kwenye kundi hilo na mahali pake pakachukuliwa na Mya Baganda na ilibainika kwamba hata hakuhusika kwenye maandalizi ya albamu “Burrn”.

Kundi hilo liliwahi kushinda tuzo kadhaa zikiwemo Pearl of Africa Music Awards, Kisima Awards za Kenya na nyingine.

Waliwahi kuteuliwa pia kuwania tuzo za Kora na Channel O.

Share This Article