Kaimu Katibu wa serikali ya kaunti ya Nairobi Patrick Analo, ametoa wito kwa bunge la kaunti hiyo kufanikisha kurejeshwa kwa mahakama za kaunti hiyo, ambazo zilipelekwa katika mahakama za Milimani na idara ya Mahakama.
Kulingana na Katibu huyo, hatua ya kuhamisha mahakama hizo imesababisha kaunti hiyo kupoteza hadi shilingi milioni 59, huku kukiwa na mzozo kati ya idara ya Mahakama na serikali ya kaunti hiyo, kuhusiana na swala hilo.
Alipokutana na wanachama wa kamati ya bunge la kaunti ya Nairobi kuhusu haki na sheria siku ya Jumatano, Analo alisema hatua ya kutokuwa na mahakama hiyo, huenda wakazi wa Jiji la Nairobi wakapuuzilia mbali sheria zinazodhibiti Jiji hilo.
Analo alidokeza kuwa mahakama hizo za hakimu ambazo zilikuwa chini ya serikali ya kaunti ya Nairobi na ambazo zilishughulikia makosa madogo madogo, zilipelekwa katika mahakama za Milimani tarehe mbili mwezi Oktoba mwaka 2023.