Rais William Ruto ameapa kufanya kila awezalo kuhakikisha anaangamiza ufisadi katika idara ya mahakama.
Amesema kamwe hatatoa hongo kwa idara hiyo kama zilivyofanya serikali zilizopita ili kupata hukumu zinazoipendelea serikali.
“Badala ya kuhongana kortini, tutamaliza ufisadi kortini,” aliapa Rais Ruto wakati akizindua ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika kaunti ya Uasin Gishu jana Jumanne.
“Ati kuna watu wengine wananiambia ati kwa sababu ile serikali ilipita, ati walikuwa na budget ya kuhongana kortini, ati mimi niende nitengeneze budget ya kuhongana kortini. Mnataka ati pesa yenu itumike kuhongana kortini? Hiyo kazi haiwezi bwana, haiwezekani. Hakuna budget itatengenezwa ya kuhonga mtu yeyote kortini. Badala ya kuhongana kortini, sisi tutamaliza ufisadi kortini,” aliongeza wakati akiwahutubia wakazi wa eneo hilo.
Ruto alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa serikali yake imedhamiria kuhakikisha mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu unafanikiwa.
Katika siku za hivi karibuni, kiongozi wa nchi ameinyoshea idara ya mahakama kidole cha lawama kwa kushirikiana na watu fulani kuhujumu utekelezaji wa mipango ya serikali, kitu ambacho ameapa hataruhusu kifanyike chini ya utawala wake.