KTCPA yapongeza mpango wa lishe shuleni

Tom Mathinji, radiotaifa and radiotaifa
2 Min Read

Chama cha wakuu wa vyuo vya mafunzo kwa walimu nchini (KTCPA),  kimeelezea imani yake kwamba mpango wa utaoji lishe kwa wanafunzi shuleni unaoungwa mkono na baraza la kitaifa la elimu kwa wanafunzi wa jamii za kuhama hama utasaidia kuimarisha mafunzo na matokeo ya mitihani katika maeneo yanayolengwa.

Mwenyekiti wa chama hicho Saul Barasa, aliusifu mpango huo akisema utaongeza idadi ya wanafunzi shuleni.

Akiongea wakati wa mkutano wa kila mwaka wa chama hicho unaoendelea jijini Mombasa, Barasa alikariri kwamba vyuo vya mafunzo kwa walimu, ndivyo hutoa mafunzo kwa walimu wa kufunza katika shule za msingi zinazonufaika na mpango wa lishe kwa wanafunzi hivyo basi chama hicho kinapania kutafuta suluhisho kwa matatizo mbali mbali yanayoikumba sekta ya elimu.

“Mpango wa lishe shuleni husaidia wanafunzi kusalia shuleni, ambapo walimu wanagenzi hupelekwa kufunzwa,” alisema Barasa.

Mpango huo wa lishe unawanufaisha wanafunzi millioni 1.2 wa shule za msingi katika sehemu kame na mitaa ya mabanda katika kaunti 11 na kaunti ndogo 85 kote nchini.

Kongamalo la kila mwaka la chama cha wakuu wa vyuo vya mafunzo kwa walimu nchini (KTCPA), limerejelewa baada ya kusitishwa kwa miaka mitatu kutokana na janga la COVID 19, likiwaleta pamoja wakuu wa taasisi za mafunzo  41 za umma na zile za kibinafsi.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article