Kituo cha ‘Dandora Hip Hop City’ cha Juliani chabomolewa

Dismas Otuke
2 Min Read

Msanii maarufu wa nyimbo za kufoka Juliani ameonyesha masikitiko yake baada ya kituo chake cha ‘Dandora Hip Hop City’ kubomolewa na tingatinga ya serikali siku ya Jumatatu.

Kituo hicho hakikusazwa na ubomozi huo unaoendelezwa na serikali katika harakati za kutunza mito kwa kuwa kilijengwa karibu na mto Nairobi.

“Huu sio mwisho bali inauma sana! Kufikiria kuwa tulikuwa tukifanya kazi ya kupanua nafasi za jirani na kuboresha kituo,” alisema Juliani kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X.

Kituo hicho kinaendesha miradi kadhaa ya kijamii ikiwemo shule ya muziki, redio ya jamii ya HipHop City FM na kituo cha kukuza biashara kwa wakazi wa Dandora wanaopenda elimu, sanaa, biashara, teknolojia, nishati mbadala na uhifadhi mazingira.

Jumapili, Juliani alifichua kwamba alipokea habari za ubomoaji huo na kuwataka mashabiki wake wasimame naye wakati huo mgumu.

“Tumepata habari kwamba kituo chetu cha kijamii, Dandora Hip Hop City kinabomolewa. Jengo lote la ghorofa 2. Ndiyo, liko karibu na mto. Tulinunua jengo hilo zaidi ya miaka 7 iliyopita,” alisema Juliani.

Mnamo Aprili 30, 2024, Rais William Ruto alitoa agizo kwa watu wanaoishi karibu na mito kuondoka ndani ya saa 48 kuanzia Mei 1.

Serikali ilichukua hatua hiyo ya kuondoa watu karibu na mito baada ya mafuriko kushuhudiwa nchini yaliyosababisha vifo vingi na kupoteza makwao hususan makazi duni.

Ni mei mosi mwaka huu ambapo Waziri wa Usalama wa kitaifa Kithure Kindiki aliagiza kubomolewa kwa majengo na nyumba zilizojengwa karibu na mito baada ya makataa ya kuondoka kwa hiari ya saa 24 kukamilika.

Share This Article