Kitabu cha Yvonne Nelson chasisimua wengi

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa Ghana Yvonne Nelson amezindua kitabu alichoandika kuhusu maisha yake kiitwacho “I Am Not Yvonne Nalson” ambacho kimesisimua wengi katika sekta ya burudani nchini Ghana na Nigeria.

Binti huyo amefichua mengi kwenye kitabu hicho kuhusu jinsi alihusiana na watu kadhaa na walivyoathiri maisha yake kwa njia nzuri na hasi.

Mrembo huyo ameangazia mahusiano yake ya kimapenzi na watu kadhaa maarufu na majaribu aliyopitia kwenye mahusiano hayo.

Katika sura mojawapo ya kitabu hicho, Nelson anasimulia uhusiano wake na mwanamuziki aitwaye Iyanya, ambapo anaelezea jinsi alihisi kusalitiwa katika kisa ambacho kinahusisha mwigizaji mwenza Tonto Dikeh.

Nelson anasema Iyanya alikuwa na tabia ya kutokuwa mwaminifu kwenye uhusiano wao ambapo alikuwa akifanya mapenzi na wanawake wengine wengi akiwemo Tonto Dikeh.

Aliamua kuonyesha kutoridhika kwake na hali hiyo kupitia mtandao wa Twitter akajibiwa na Dikeh ambaye alikubali kuingilia uhusiano wao na kumwambia kwamba watu hubadilika na hisia zao pia hubadilika kwa hivyo aendelee na maisha yake.

Sura ya 14 ameipa mada ya “Genevieve Nnaji na wengine” ambapo anasimulia alivyokutana na mwigizaji huyo wa hadhi ya juu huku sura ya 20 ikizamia swala la vipimo vya vinasaba au ukipenda DNA na watoto wa Peter Ala Adjetey aliyekuwa wakili na mwanasiasa nchini Ghana, akijaribu kutafuta ukweli kuhusu babake mzazi.

Adjetey alihudumu kama spika wa bunge la Ghana kati ya mwaka 2001 na 2005.

Kitabu hicho kimezungumziwa na kinaendelea kuzua gumzo katika ulingo wa burudani hata ingawa wengi hawajakitia mikononi.

Sehemu za kitabu hicho zimepachikwa kwenye mitandao ya kijamii.

Wengi sasa wanakisia tu kuhusu mengine mengi ambayo Yvonne Nelson amefichua kwenye kitabu hicho.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *