Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni ameagiza kufungwa kwa kisima kimoja katika kaunti ya Kisii kinachoaminika kuwa chanzo cha ugonjwa usiojulikana.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa, kisima hicho ambacho kimetumika kwa muda, kilikuwa kimechanganyika na kinyesi.
Muthoni amesema hakuna sababu ya kuhofu na kisima hicho kitafungwa kwa muda wakati uchunguzi zaidi ukiendelea kuhusiana na ugonjwa huo.
Kisima hicho kimekuwa chanzo cha masaibu ya wakazi wa vijiji vitatu katika kaunti ya Kisii ambao wameugua ugonjwa usiojulikana uliowafanya kuendesha.
Wakati wa ziara yake katika kaunti ya Kisii leo Jumanne, Katibu Muthoni alikutana na Naibu Gavana wa Kisii Elijah Obebo na kamishna wa kaunti hiyo Joseph Kibet.
Wote hao walizungumzia juhudi zinazoendelea za kuimarisha utekelezaji wa sera ya afya kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo.
“Mazungumzo yetu yaliangazia hatua za dharura za kudhibiti mlipuko huo, ikiwa ni pamoja na mikakati ya dharura ya kukabiliana na ugonjwa huo, uboreshaji wa afya ya umma na kuimarisha mifumo ya uangalizi wa ugonjwa,” alisema Muthoni baada ya mkutano huo.