Bingwa mara tatu wa olimpiki wa mbio za mita 1500, Faith Kipyegon, amethibitisha kushiriki makala ya nne ya msururu wa mbio za nyika duniani za Absa Sirikwa Classic, zitakazoandaliwa Jumamosi hii eneo Lobo mtaani Kapseret jijini Eldoret.
Kipyegon, ambaye pia ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mita 5,000 na maili moja, atarejea kwa mashindano ya Sirikwa kuwinda taji ya komita 10 aliyotwaa mwaka 2023 kwenye makala ya pili.
Kipyegon hata hivyo atakabiliana na wanariadha wengine mahiri wakiwemo mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kilomita 10 na pia mwanariadha mwenye kasi sana kati katika mbio za kilomita 21 Agnes Jebet Ng’etich, na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya marathoni Ruth Chepng’etich.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 31 alifungua msimu wake wa mwaka 2023 kwa kushinda mbio za sirikwa, kabla ya kushinda dhahabu za dunia za mita 1,500 na 5,000 kwenye mashindano ya dunia mjini Budapest baadaye mwaka huo.
Mshindi wa nishani ya fedha ya dunia ya mita 5,000 mwaka 2022, Stanley Waithaka ataongoza mbio za wanaume huku bingwa wa olimpiki katika mita 800, Emmanuel Wanyonyi, akilenga kutetea taji ya mbio za kilomita mbili.
Mashindano hayo ya Jumamosi yatawashirikisha wanariadha matata kutoka mataifa ya Ethiopia, Uganda, Tanzania, na mataifa ya ulaya.
Zaidi ya wanariadha 500 wa humu nchini wametoa ithibati kushiriki katika vitengo vya chipukizi chini ya umri wa miaka 20, zikiwa kilomita 6 wanawake na kilomita 8 wanaume, kilomita 10 wanaume na wanawake, na kilomita 2 mzunguko mmoja kwa wanaume na wanawake.
Washindi wa kilomita 10 watatuzwa shilingi 780,000, washindi wa medali za fedha laki sita unusu, huku watakaonyakua nishani za shaba wakituzwa 520,000.