Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za marathoni Kelvin Kiptum amezikwa leo Ijumaa nyumbani kwake eneo la Naiberi, kaunti ya Uasin Gishu kwenye mazishi yaliyoongozwa na Rais William Ruto.
Rais Ruto ameahidi kujenga nyumba nyingine kwa familia ya marehemu na kumpa kazi mjane wa mwanariadha huyo.
Akihutubu katika ibada iliyoandaliwa katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Chepkorio, kaunti ya Elgeyo Marakwet, Ruto alitoa changamoto kwa wanariadha wote watakaoiwakilisha Kenya kwa michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa mwaka huu kusajili matokeo bora kama njia ya kumuenzi marehemu Kiptum.
Awali, kulikuwa na msafara mkubwa wa magari na watu waliosindikiza mwili wa marehemu kutoka makafani ya Elgeyo Marakwet hadi uwanja wa Chepkorio kulikoandaliwa ibada.
Mamia ya wanariadha waliotoa risala walimlimbikizia sifa kedekede marehemu, wakiwemo mabingwa wa dunia Faith Kipyegon, Mary Moraa, Julius Yego na bingwa wa dunia mwaka 2013 Milcah Chemos na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mita 800 David Rudisha miongoni mwa wengine.
Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Riadha Duniani Sebastien Coe.
Marehemu Kiptum amemwacha mjane na watato wawili.