Mwanamuziki wa Uganda King Saha amezindua kibao kipya kwa jina “Wewe” ambalo ni neno la Kiswahili hata ingawa wimbo wenyewe ni wa lugha ya Luganda.
Alizindua kazi hiyo alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha After 5 ambapo alizungumzia pia tamasha anayoandaa ya mwezi Agosti katika uwanja wa Kololo jijini Kampala.
King Saha ambaye jina lake halisi ni Ssemanda Manisul, alisema kwamba anashughulikia maandalizi ya tamasha hiyo yeye binafsi.
Mmiliki huyo wa kampuni ya Kings Love Entertainment, anaamini kwamba kuhusika katika maandalizi hayo kutahakikishia mashabiki zake ubora wa hali ya juu.
“Ninasimamia maandalizi ya tamasha, kama kawaida. Njoo muunge mkono tamasha! Zamu hii tunaleta burudani Kololo na onyesho litakuwa la viwango vingine,” alisema mwimbaji huyo wa asili ya Entebbe.
Nia ya King Saha ya kusimamia tamasha hiyo yeye mwenyewe inaonyesha kujiamini kwake na kujitolea kuhakikisha anawapa mashabiki burudani ya kiwango cha juu.
Kwa miaka mingi, mwimbaji huyo amejijengea sifa nzuri kwa kutoa maonyesho yenye nguvu na ya kusisimua, huku akiweza kuungana kwa karibu na hadhira yake.
Tangazo hilo tayari limezua msisimko mkubwa miongoni mwa mashabiki wake, wengi wao wakihesabu siku zilizosalia kabla ya tukio hilo kufanyika.
Huku maandalizi yakiwa yanaendelea kwa kasi, tamasha la King Saha litakalofanyika Kololo linaonekana kuwa moja ya matukio makubwa ya muziki katika kalenda ya burudani nchini Uganda mwaka huu.