Jua Kali yashinda tamasha ya filamu ya Diani 2026

Kufuatia ushindi huo, mwandaaji Joash Omondi alituzwa zawadi ya shilingi 100,000 pesa za Kenya

Marion Bosire
2 Min Read

Filamu fupi kwa jina ‘Jua Kali’, iliyoandaliwa na Joash Omondi, imetwaa tuzo ya Filamu Bora Fupi ya Afrika katika awamu ya pili ya tamasha ya filamu ya Diani.

Kufuatia ushindi huo, Omondi alichukua zawadi ya shilingi 100,000 pesa za Kenya.

Tuzo hiyo ilitolewa na waandaaji wa tamasha kwa kutambua ubora wa simulizi na umahiri wa kisanaa katika utengenezaji wa filamu.

Tuzo ya Filamu Bora Fupi ya Kimataifa ilinyakuliwa na Les Âmes du Fouta, iliyoandaliwa na Alpha Diallo, ambaye pia alizawadiwa shilingi 100,000 za Kenya.

Mashindano ya Filamu Fupi za Afrika ya mwaka huu yaliongozwa na mtayarishaji filamu mashuhuri Martin Scorsese kama Rais wa Jopo la Majaji, yakionyesha utofauti, ubunifu na utajiri wa simulizi za Kiafrika.

Akizungumza katika tamasha hiyo, Kamishna wa Tume ya Filamu Kenya, Ilham Tasir, alisisitiza umuhimu wa tamasha za filamu katika kujenga hadhira, kuibua fursa kwa watengenezaji wa filamu na kuimarisha uchumi wa sekta ya ubunifu nchini.

Waandaaji walipongeza washindi kwa kuwasilisha simulizi halisi na zenye mvuto zinazoakisi maisha na uzoefu wa Waafrika.

Tamasha ya filamu ya Diani pia ilisifiwa kwa kuendelea kutoa jukwaa linalowezesha watengenezaji filamu wa Afrika, kukuza sauti za Waafrika na kuitangaza hadithi za bara hili kwa hadhira ya kimataifa huku ikihamasisha kizazi kijacho cha wabunifu.

Share This Article