CCFR yaandaa mpango wa kufaidi wabunifu nchini Rwanda

Hili ni dhihirisho la jukumu linalozidi kukua la CCFR zaidi ya kukuza lugha ya Kifaransa, kwa kuifanya kuwa kitovu cha ushirikiano wa kisanii, kubadilishana tamaduni na maendeleo ya kitaaluma.

Marion Bosire
2 Min Read
Aurélie Royet-Gounin, Balozi wa Ufaransa nchini Rwanda na Rais Paul Kagame

Kituo cha Utamaduni wa Ufaransa nchini Rwanda, CCFR kimetangaza mpango wa kitamaduni wa miezi miwili ambao utafaidi wabunifu nchini Rwanda.

Mpango huo utaanza Julai Mosi hadi Agosti 29 na washiriki watafaidi kutokana na tamthilia, filamu, mitindo ya mavazi, muziki, dansi, maonyesho ya sanaa na shughuli zinazolenga vijana, pamoja na mipango iliyoundwa kuimarisha sekta ya ubunifu nchini Rwanda.

Hili ni dhihirisho la jukumu linalozidi kukua la CCFR zaidi ya kukuza lugha ya Kifaransa, kwa kufanya kituo hicho kuwa kitovu cha ushirikiano wa kisanii, kubadilishana tamaduni na maendeleo ya kitaaluma.

Hatua hizo zitaafikiwa kupitia maonyesho, warsha, tamasha na maonesho yanayowashirikisha wasanii wa ndani na wa kimataifa.

Washiriki wa mpango huo watajifunza mengi ikiwemo lugha ya Kifaransa na usimulizi wa hadithi, tamthilia, dansi, michezo na shughuli nyingine za ubunifu.

CCFR imefichua tena ujio wa mradi mwingine wenye kauli mbiu ya “Shaping Future: Renforcer les Industries Créatives du Rwanda” ambao utadumu miezi 30.

Mradi huo unalenga kushughulikia upungufu wa ujuzi, changamoto za upatikanaji wa masoko na changamoto za ufadhili zinazokabili sekta ya ubunifu nchini Rwanda kupitia mafunzo maalumu, programu za makazi ya wasanii, ruzuku za usafiri na msaada wa ujasiriamali.

Waandaaji wanatarajia kuwafundisha zaidi ya wataalamu 375 wa sekta ya ubunifu huku wakichangia lengo la Rwanda la kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa (GDP) hadi asilimia tano ifikapo mwaka 2030.

Share This Article