Kindiki: Vitisho vya mwaka 2023 ndivyo vya mwaka 2024

Marion Bosire
1 Min Read
Waziri wa Usalama Prof. Kithure Kindiki.

Waziri wa usalama wa taifa Profesa Kithure Kindiki amesema kwamba tathmini ya wizara yake inaonyesha kwamba vitisho vilivyokabili wakenya mwaka 2023 vitasalia mwaka huu wa 2024.

Kwenye taarifa ya kutamatisha mwaka aliyotoa waziri huyo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, alitaja ugaidi, ujambazi, mihadarati, ufisadi, virugu, mashambukizi ya mitandaoni na mabadiliko ya tabianchi kuwa vitisho vikuu vya mwaka jana.

Huku akiutaja mwaka huo kuwa mgumu zaidi, Kindiki alisema kwamba wizara yake imejitolea kikamilifu kuhakikisha usalama wa wananchi.

Kindiki alisema kwa bahati mbaya baadhi ya mipango ya wahalifu ilifanikiwa na kusababisha madhara na kwamba baadhi ya visa hivyo vilitangazwa na vinafahamika.

Alifafanua kwamba usalama wa ndani ni zaidi ya visa vilivyotapakaa vya wahalifu kufanikiwa kudhuru wananchi.

“Usalama wa ndani unahusu sana visa vingi visivyoripotiwa vya kukabiliwa na kuangamizwa kwa magaidi, kukandamiza majambazi, kuharibu mipango ya uhalifu na kuzuia kushambuliwa kwa miundomsingi muhimu.” Alisema Kindiki kwenye taarifa hiyo.

Alishukuru maafisa wote wa usalama waliojitolea kuhakikisha usalama nchini huku akiwatakia wao pamoja na familia zao baraka, neema na afya njema mwaka huu wa 2024.

Share This Article