Mfumo mpya wa Bima ya Afya ya Jamii, SHIF utahakikisha Wakenya wengi zaidi iwekezanavyo wanapata huduma bora na za gharama nafuu za matibabu.
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki anasema utekelezaji wa mfumo huo pia utaondoa hali ilivyokuwa chini ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya, NHIF iliyowanufaisha watu na watoaji huduma wachache.
Prof. Kindiki aliyasema hayo wakati alipofanya mkutano wa mashauriano na uongozi wa Wizara ya Afya katika makazi yake mtaani Karen jijini Nairobi leo Jumanne ili kuangazia hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa bima mpya ya afya ya SHIF.
Aidha, wakati wa mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa na Makatibu Mary Muthoni na Harry Kimtai, changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa SHIF zilijadiliwa sawia na namna ya kuzitatua.
Mkutano huo unakuja wakati Wakenya wengi wamelalamikia changamoto nyingi wanazokumbana nazo katika kupata huduma za matibabu chini ya mfumo huo.
Serikali imekiri kuwepo kwa changamoto hizo lakini inasema inachukua hatua za haraka kuzisuluhisha.
Hadi kufikia sasa, Wakenya zaidi ya milioni 25 wamejisajili kwenye bima ya SHIF.