Mabadiliko ya tabia nchi ni moja ya matishio makuu matano yanayoikumba nchi hii.
Matishio mengine ni pamoja na ugaidi, wizi wa mifugo, matumizi ya pombe haramu na dawa za kulevya pamoja na itikadi kali za kidini na za kisiasa.
Kulingana na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki, mizozo ya kila mara kati ya wakulima na wafugaji wa kuhamahama inatokana na upiganiaji wa rasilimali chache ambazo uhaba wake unasababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Anasema upiganiaji wa rasilimali hizo mara nyingi husababisha vifo, majeraha na uharibifu wa mali.
“Tuko na wajibu binafsi na wa pamoja wa kizalendo kutunza mazingira na kubadilisha hali hiyo kupitia upanzi wa miti,” alisema Prof. Kindiki alipoongoza zoezi la kitaifa la upanzi wa miti katika kaunti ya Garissa leo Jumatatu.
Waziri Kindiki anasema upanzi wa miti utakuwa utamaduni wa kitaifa nchini na maafisa wote wa utawala wa serikali ya kitaifa wanahimizwa kuongoza mazoezi ya upanzi wa miti katika maeneo yao.
Anasema hatua hiyo itasaidia mno kuikinga nchi hii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na ukame na mafuriko.
Miti zaidi ya 300,000 ilikusudiwa kupandwa katika eneo la Kaskazini Mashariki huku miti 100,000 ikilengwa kupandwa katika kila kaunti za Garissa, Mandera na Wajir.